Jumatatu 2 Novemba 2026 - 01:15
Jumuiya ya Al-Wifaq ya Bahrain Yalaani Hukumu ya Kifo Dhidi ya Sheikh Hussein Ma'tuq na Kuitaka Serikali ya Kuwait Iifute

Hawza/ Jumuiya ya Kitaifa ya Kiislamu ya Al-Wifaq ya Bahrain imelaani hukumu ya kifo iliyotolewa na mahakama za Kuwait dhidi ya Ayatullah Sheikh Hussein Ma'tuq na watu wengine wawili, ikiitaja kuwa ni hukumu isiyozingatia misingi ya uadilifu na haki. Jumuiya hiyo imetoa tahadhari kwamba hatua hiyo ni ongezeko hatari linalotishia utulivu na kuishi pamoja na kwa amani katika jamii ya Kuwait.

Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Jumuiya ya Kitaifa ya Kiislamu ya Al-Wifaq ya Bahrain, katika kulaani hukumu ya kifo iliyotolewa na mahakama za Kuwait dhidi ya Ayatullah Sheikh Hussein Ma'tuq na watu wengine wawili, imetangaza kwamba hukumu hiyo imetolewa kufuatia kesi iliyokosa misingi ya uadilifu na haki.

Katika taarifa yake, Jumuiya ya Al-Wifaq imesema kuwa; hukumu hiyo inaashiria ongezeko hatari la mvutano ambalo linaweza kutishia kuishi pamoja kwa amani na utulivu nchini Kuwait. Hii ni kwa sababu uamuzi huo una athari kubwa za kisiasa na kijamii, zinazolenga uhuru wa raia, faragha ya masuala yao ya kidini na utekelezaji wa ibada zao za kidini. Aidha, uamuzi huo unawalenga pia watu mashuhuri katika nyanja za elimu na dini.

Jumuiya hiyo imebainisha kuwa; Sheikh Ma'tuq ni miongoni mwa viongozi mashuhuri wa Kiislamu na kitaifa katika eneo la Ghuba ya Uajemi, anayejulikana kwa msimamo wake wa kupenda amani na misimamo yake inayolenga kulinda maslahi ya kitaifa na kudumisha utulivu. Taarifa hiyo imesisitiza kwamba; Sheikh huyo hakuwahi kutafuta makabiliano wala kuvuruga usalama, bali amelengwa kwa tuhuma za hila na udanganyifu.

Jumuiya ya Al-Wifaq imehusisha kuongezeka hatua za kiusalama nchini Kuwait na hatua zinazofanana na hizo nchini Bahrain. Imesema kuwa hali ya kisiasa, kiusalama na kijeshi inayotawala eneo hili inatumiwa vibaya ili kufanikisha malengo ya kisiasa dhidi ya wapinzani wa ndani, kupitia mashambulizi ya propaganda, kupotosha ukweli na kampeni za kuchafua taswira ya watu.

Jumuiya hiyo imezitaka mamlaka za Kuwait kuiondoa hukumu ya kifo, kusitisha mashambulizi ya kiusalama dhidi ya raia wa Kishia na kurejesha utaratibu katika maisha ya kisiasa kwa kuzirejeshea taasisi za kikatiba hadhi na mamlaka yake. Aidha, Al-Wifaq imetoa tahadhari kuhusu matokeo ya kuimarishwa utawala wa kimabavu na uingiliaji wa mataifa ya kigeni katika mchakato wa kudhoofisha umoja wa kitaifa na utulivu.

Mwisho, Jumuiya ya Al-Wifaq imesisitiza kwamba; viongozi wa kitaifa na Kiislamu, akiwemo Sheikh Ma'tuq, ni miongoni mwa nguzo zinazohakikisha jamii zinalindwa dhidi ya fitina na migogoro ya ndani. Jumuiya hiyo imezitaka mamlaka badala ya kuwazunguka kwa vikwazo na kuwalenga viongozi hao, zitumie na kunufaika na nafasi yao katika kulitumikia taifa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha